Chapter 1.1 (Kiswahili 8)

Kusikiliza na Kuzungumza: Maamkuzi

Maamkuzi

Jerono: Sabalkheri Bwana Koti. U hali gani?

Koti: Sabalkheri Jerono. Mimi ni mzima na buheri wa afya. Je, wewe?

Jerono: Ahoo! Mimi pia ni mzima kama kigongo. Alhamdulilahi! Namshukuru Rabili alamina Mola wa ulimwengu wote.

Koti: Nyumbani watu waambaje?

Jerono: Ni wazima pia. Hawana la kuamba.

ZOEZI

  1. Igizeni mazungumzo ya Jerono na Koti.
  2. Igizeni mazungumzo yanayotumia maamkuzi haya:
    1. Masalkheri
    2. Asalaam Aleikum
    3. Sabalkheri
    4. Mwambaje?
    5. U mzima?

Kusoma: Ufahamu

Kuna masuala nyeti yanayohusu elimu nchini. Masuala hayo ni kama vile elimu ya bure, elimu kwa wote, elimu ya watoto wadogo na vilevile suala la jinsia.

Elimu ya bure kwa watoto wote wa shule za msingi za umma ilianza kutolewa mwaka wa 2003. Hapo awali elimu ilitolewa kwa kugawana gharama ambapo wazazi waligharamia elimu ya watoto wao. Jukumu la serikali lilikuwa kulipa walimu tu.

Gharama ya elimu iliwafanya wazazi wengi kushindwa kuwapeleka watoto wao shuleni. Baadhi ya waliofanikiwa kuingia shuleni walishindwa kumaliza masomo hadi darasa la nane.

Tangu serikali ianze kutoa elimu bila malipo idadi ya wanaojiunga na shule imeongezeka sana. Watoto wengi sasa wanasoma na kukamilisha darasa la nane. Serikali huwahimiza wazazi wote wapeleke watoto wao shuleni. Huko shuleni wanapata vitabu, kalamu, madaftari na nyenzo nyingine nyingi zilizolipiwa na serikali. Jukumu la mzazi sasa ni kumpeleka mtoto wake shule tu na kuhakikisha kuwa anapata chakula cha kutosha na sare za shule.

Elimu bila malipo imechangia kutimiza azma ya elimu kwa wote. Watoto wenye umri mkubwa waliokuwa hawasomi pamoja na baadhi ya wazee wameamua kujinufaisha na elimu hii kwa kujiunga na shule.

Ukweli ni kuwa, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, ndiyo sababu serikali inatilia mkazo elimu ya watoto wadogo. Shule zote za chekechea au za nasari zilizo za umma zatakiwa ziwe chini ya shule ya msingi iliyo karibu ili zishughulikiwe kiutawala. Walimu wa shule hizo sasa wanapewa mafunzo na serikali ili kuwaimarisha. Shule hizo hukaguliwa na wakaguzi wa Wizara ya Elimu mara kwa mara.

Watoto wa jinsia zote mbili – wasichana na wavulana – wanahimizwa kusoma. Hivi sasa idadi ya wasichana walio shuleni ni kubwa sana ikilinganishwa na hapo awali. Wanasoma sambamba na wavulana.

Hata hivyo, hakuna masika yasiyokuwa na mbu. Kuna matatizo yanayotishia elimu bila malipo nchini. Mambo mawili yanayotatiza juhudi za serikali mno katika kutoa elimu ni ugonjwa wa UKIMWI na umaskini. UKIMWI umefanya pawe na idadi kubwa ya watoto yatima. Mayatima hukabiliwa na matatizo chungu nzima katika malezi yao kama vile lishe bora, makazi na mavazi. Idadi ya walimu wanaolemewa na kazi au kuaga dunia kutokana na janga hili pia ni tisho katika utoaji wa elimu.

Umaskini unaokumba wananchi wengi unawafanya washindwe kuelimisha watoto wao zaidi wanapofuzu darasa la nane. Hata hivyo, serikali imeshughulikia suala hili kwa kuanzisha elimu bila malipo katika shule za upili za kutwa.

MASWALI

  1. Taja masuala manne yanayohusu elimu nchini.
  2. Utaratibu wa kugawana gharama ya elimu baina ya wazazi na serikali uliondolewam waka gani?
  3. Je, kugawana gharama kulikuwa na faida ama hasara? Eleza.
  4. Ni manufaa gani ambayo yamepatikana kutokana na elimu kugharamiwa na serikali?
  5. Jukumu la mzazi sasa ni lipi?
  6. Taja matatizo mawili yanayokumba juhudi za kutoa elimu nchini.
  7. Neno UKIMWI ni kifupi cha maneno gani?
  8. Ni nini maana ya methali: Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo?
  9. Ipe kichwa kifaacho taarifa hii.
  10. Tunga sentensi ukitumia maneno haya:
    1. Umma
    2. Jukumu
    3. Nyenzo
    4. Azma
Please wait