Chapter 1.1 (Kiswahili 7)

Kusikiliza na kuzungumza: Kusikiliza na kujibu

Kusikiliza na kujibu

Kichocheo

  1. Je, unaposikiliza mtu akizungumza unafaa kufanya nini ili uupate ujumbe kikamilifu?
  2. Unapomjibu mtu katika mazungumzo, unazingatia mambo gani ili akuelewe vilivyo?

Shughuli ya 1

Vipengele vya kuzingatia katika usikilizaji wa mazungumzo

  1. Tazama picha hii
Simba anazungumza na Mnyama Mgeni
  1. Mweleze mwenzako kuhusu picha uliyoitazama. Unaweza kuongozwa na maswali haya:
    1. Unafikiri ni kwa nini Simba ameshika pua yake?
    2. Ni ishara gani inayoonyesha kuwa Mnyama Mgeni anamsikiliza Simba kwa makini?
    3. Unafikiri ni kwa nini Simba wameangaliana ana kwa ana na Mnyama Mgeni?
    1. Sikilizeni mazungumzo kati ya Simba na Mnyama Mgeni ambayo mwalimu atawasilisha.
    2. Taja vitendo ambavyo wanyama walifanya kuonyesha kuwa walikuwa wanasikiliza wakati wa mazungumzo yao.
    3. Eleza umuhimu wa vitendo vifuatavyo unapomsikiliza mwenzako:
      1. kusikiliza kwa makini
      2. kumtazama mzungumzaji
      3. kutikisa kichwa
      4. kutumia vihisishi
      5. kuepuka vizuizi vya mawasiliano.
Mazungumzo ya wanyama

Shughuli ya 2

Vipengele vya kuzingatia katika kujibu mazungumzo

Ukiwa na mwenzako:

  1. Jadilini tabia za kinidhamu alizozingatia Mnyama Mgeni wakati wa kumjibu Simba.
  2. Mweleze kwa nini ni muhimu kuzingatia tabia zifuatazo wakati wa kumjibu mtu katika mazungumzo:
    1. kutumia lugha ya adabu
    2. kutomkata kalima mzungumzaji
    3. ubadilishanaji zamu ufaao
    4. kujibu kwa kujikita katika kiini cha swali.

Shabashi!

Nimegundua kuwa kuna mambo muhimu ya kuzingatia katika mawasiliano ili kuwe na maelewano. Mambo hayo ni kama vile, kusikiliza kwa makini, kumtazama mzungumzaji, kutikisa kichwa, kutumia vihisishi na kuepuka vizuizi vya mawasiliano.

Shughuli ya 3

Vipengele vifaavyo katika kusikiliza na kujibu mazungumzo

  1. Mkiwa wawiliwawili, zungumzieni kuhusu usafi wa mwili mkizingatia:
    1. kusikiliza kwa makini
    2. kumtazama mzungumzaji kwa makini ili upate ishara za uso
    3. kutikisa kichwa ili kuonyesha kukubaliana na kauli
    4. kutumia maneno au vihisishi vya kuhimiza kuendelea kuzungumza kama vile ehee!
    5. kuepuka vizuizi vya mazungumzo
    6. kutumia lugha ya adabu
    7. kutomkata kalima mzungumzaji
    8. kubadilishana zamu ifaavyo wakati wa mazungumzo
    9. kujibu kwa kujikita katika kiini cha swali.

Changamkia

Igiza mazungumzo ya simu na mwenzako. Zungumzieni kuhusu usafi wa kibinafsi.

Tembea na majira

Mkiwa katika kikundi:

  1. Tumieni vifaa vya kidijitali kama vile simu, tabuleti au kipakatalishi kutafuta na kusikiliza video ya mazungumzo mtandaoni kuhusu usafi wa kibinafsi.
  2. Tambueni vipengele vifaavyo vya kusikiliza na kujibu mazungumzo katika video hiyo.

Shirikisha mzazi au mlezi

  1. Ukiwa na mzazi au mlezi wako, zungumzieni kuhusu namna ya kutunza vifaa vinavyotumika katika usafi wa kibinafsi.
  2. Zingatia vipengele vifaavyo katika kusikiliza na kujibu mazungumzo.
Please wait