Chapter 1.1 (Kiswahili 7)

Kusikiliza na Kuzungumza: Maamkuzi

Maamkuzi

Hapa ni shuleni. Watu hawa wanafanya nini?
Mwalimu na mwanafunzi wamekutana

Mwalimu na mwanafunzi wanaamkuana.

Mwanafunzi anasema: “Waambaje mwalimu?”
​Mwalimu anajibu: “Sina la kuamba.”
​Mwalimu anaendelea kusema: “U hali gani?”
​Mwanafunzi anajibu: “Sijambo mwalimu.”
​Kisha mwalimu anauliza: “Habari ya nyumbani?”
​Naye mwanafunzi anajibu: “Nyumbani tu salama.”

Baadaye mwalimu atakapowaaga wanafunzi jioni atasema: “Alamsiki.”
​Wanafunzi nao watamjibu: “Binuru.”
​Kisha, mwalimu atawaambia: “Tutaonana kesho.”
​Nao wanafunzi watajibu: “Inshallah”.

Maana ya Inshallah ni ‘Mwenyezi Mungu akipenda.’ Maamkuzi kama haya hudhihirisha adabu na heshima miongoni mwa watu katika jamii.

Zoezi

1. Jibu maamkizi yafuatayo:

  1. Je, salama? 
  2. Mwambaje? 
  3. Habari za utokako? 
  4. Kwaheri. 
  5. Umeamkaje? 
  6. Umeshindaje? 
  7. Hujambo?
  8. Hamjambo?
  9. Habari za jioni?
  10. Sabalkheri!
  11. Lala salama/unono!
  12. Nyumbani hakujambo?
  13. Kaka ameshindaje?
  14. M hali gani?
  15. Masalkheri!

2. Igizeni maamkuzi ya mwalimu na mwanafunzi.

Maelezo zaidi

Neno nashukuru hutumika katika maamkuzi. 
Kwa mfano:

  1. Ulilalaje? — Nililala vyema, nashukuru.
  2. Umeamkaje? — Nimeamka vizuri, nashukuru.

Shukrani hizi huwa ni kwa Mwenyezi Mungu.

Please wait